Yesu Kristo Mzaliwa wa Kwanza, Nini Maana Yake?

YESU KRISTO MZALIWA WA KWANZA, NINI MAANA YAKE?

Biblia katika maeneo mbalimbali ya vitabu vya agano jipya inamtaja Yesu kristo Bwana wetu kuwa ni mzaliwa wa Kwanza, Maeneo haya ni kama yafuatayo.

WARUMI

8.28  Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake.

8.29  Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.

8.30  Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza.

WAKOLOSAI

1.13  Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake;

1.14  ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi;

1.15  naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.

1.16  Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake.

1.17  Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye.

1.18  Naye ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote.

WAEBRANIA

1.5  Kwa maana alimwambia malaika yupi wakati wo wote, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa? Na tena, Mimi nitakuwa kwake baba, Na yeye atakuwa kwangu mwana?

1.6  Hata tena, amletapo mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, asema, Na wamsujudu malaika wote wa Mungu.

UFUNUO

1.4  Yohana, kwa yale makanisa saba yaliyoko Asia; Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwake yeye aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja; na zitokazo kwa roho saba walioko mbele ya kiti chake cha enzi;

1.5  tena zitokazo kwa Yesu Kristo, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake,

1.6  na kutufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa Mungu, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina.

Baada ya kusoma maeneo hayo swali huja kwa waamini kwamba, Nini maana ya Yesu kuwa mzaliwa wa kwanza?

WAKOLOSAI 1:18 NA UFUNUO 1:5

Katika Maeneo hayo matano yanayomtaja Yesu kuwa ni mzaliwa wa kwanza maeneo mawili yanaunganisha uzaliwa wa kwanza wa Yesu na kifo yaani yanaonyesha uzaliwa huu wa kwanza ni cheo baada ya kifo. Wakolosai 1:18 Inamuita Yesu “Mzaliwa wa kwanza katika wafu” ili awe mtangulizi katika yote. Ufunuo 1:5 inamuita “Mzaliwa wa Kwanza wa waliokufa”. Hivyo ni dhahiri kwamba Yesu anaitwa mzaliwa wa kwanza ikimaanisha ndiye mwanadamu wa kwanza kufufuka (Baada ya kufa) na kuwa mtangulizi wa kuishi maisha mapya ya ulimwengu mpya ambayo waliokufa katika Yesu watakapofufuliwa watayaishi. Unaweza kujiuiza inakuwaje Yesu anakuwa mtangulizi wakati kuna watu walifufuka kabla yake yeye?. Mfano ni Lazaro ambaye alifufuliwa na Yesu mwenyewe. Jibu ni kwamba waliofufuliwa kabla ya Yesu walirudi katika miili yao ya kawaida sio katika miili ya Utukufu na pia walirudi kuishi maisha yao hapa duniani na mwisho wakafa tena. Lazaro alifufuliwa na Yesu lakini hakufufuka na mwili wa utukufu na alikufa tena baadaye. Lakini Yesu alifufuka na mwili wa utukufu na hafi tena hivyo yeye ndiye mwanadamu wa kwanza kufa na kufufuka katika mwili wa utukufu ambao watakatifu wote wataupata siku yeye atakaporudi mara ya pili. Kuhusu mwili wa utukufu watakatifu watakaoupata Paulo anaandika akisema

1 WAKORINTHO

15.51 Angalieni, nawaambia ninyi siri; hatutalala sote, lakini sote tutabadilika,

15.52  kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana parapanda italia, na wafu watafufuliwa, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika.

15.53  Maana sharti huu uharibikao uvae kutokuharibika, nao huu wa kufa uvae kutokufa.

15.54 Basi huu uharibikao utakapovaa kutokuharibika, na huu wa kufa utakapovaa kutokufa, hapo ndipo litakapokuwa lile neno lililoandikwa, Mauti imemezwa kwa kushinda.

Hii ndio maana maeneo mengine Biblia inamuita Yesu LIMBUKO LA WALIOLALA Ikimaanisha yeye ni mtangulizi katika kufufuka. Limbuko ni mazao ya kwanza yanayopatikana katika kilimo na kutolewa kwa Mungu kama uhakikisho kwamba mavuno mengine yatapatikana. Hivyo Yesu ndie mwanadamu wa kwanza kufufuka katika wafu na kuingia katika Maisha ndani ya mwili wa utukufu nay eye ndiye uhakikisho kwamba jambo hilo litatokea kwa waamini wote.

1 WAKORINTHO 15

15.20  Lakini sasa Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala.

15.21  Maana kwa kuwa mauti ililetwa na mtu, kadhalika na kiyama ya wafu ililetwa na mtu.

15.22  Kwa kuwa kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa.

15.23  Lakini kila mmoja mahali pake; limbuko ni Kristo; baadaye walio wake Kristo, atakapokuja.

Hivyo Yesu anapoitwa Mzaliwa wa kwanza katika wafu/kwa waliokufa Katika WAKOLOSAI 1:18 na UFUNUO 1:5  ni sawa na kumwita limbuko la waliolala. Hii yote ikiwa na maana YEYE NDIYE MWANADAMU WA KWANZA KUFUFUKA (BAADA YA KUFA) NA KUWA MTANGULIZI WA KUISHI MAISHA MAPYA YA ULIMWENGU MPYA AMBAYO WALIOKUFA KATIKA YESU WATAKAPOFUFULIWA WATAYAISHI/WAAMINI WOTE WATAYAISHI BAADA YA YESU KURUDI TENA.

WAKOLOSAI 1:15

Pamoja na kwamba wakolosai 1:15 iko kwenye aya moja na 1:18 lakini matumizi ya neno mzaliwa wa kwanza yanatofautiana kidogo. Katika 1:15 Yesu anatajwa kwa sifa zake mbili: ya kwanza yeye ni mfano/picha ya Mungu asiyeonekana (Sawa na Yohana 1:1,18 na Waebrania 1:3), na sifa ya pili yeye ni mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Yeye ni mzaliwa wa kwanza kwa maana ya kwamba yeye ni Mkuu juu ya viumbe vyote. Kwa nini yeye ni Mkuu juu ya viumbe vyote? Ni kwa sababu katika yeye vitu vyote viliumbwa (1:16), yeye alikuwepo kabla ya vitu vyote (1:17a) na yeye ndiye anayevishikilia vitu vyote (1:17b).

Je ukuu wake unaweza kumaanisha kwamba Yesu ni kiumbe wa kwanza?

Jibu la moja kwa moja ni hapana, Biblia haijasema yeye ni kiumbe wa kwanza na mara nyingine Bibia inapotumia neno hili mzaliwa wa kwanza katika lugha ya picha huwa inazungumzia ubora na sio kutangulia. Mfano, Mungu anamwambia farao kwamba Israeli ni mzaliwa wake wa kwanza (Kutoka 4:22). Hii inamaanisha kwamba Israeli wanahesabiwa kuwa ni bora kulinganisha na mataifa mengine.

WARUMI 8:29

Warumi 8:29 “Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi.”

Warumi 8:29 inaelezea uzaliwa wa kwanza wa Yesu katika kuhusiana na kufa na kufufuka japo haijasema moja kwa moja kama wakolosai 1:18 na Ufunuo 1:5. Swali ni kwa namna gani?

Warumi inasema Mungu aliwachagua tangu asili waamini ili wafananishwe na mfano/picha wa mwana wake ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Kwa muktadha huu Paulo anamtaja Yesu kama ndiye picha halisi ya waamini watakavyokuwa baada ya ukamlisho wa kazi ya ukombozi. Na kwa kusoma maeneo mengine ya Biblia tunatambua kwamba waamini watakuwa kama Yesu baada ya wao kufufuliwa/kubadilishwa wakati wa ujio wa Yesu mara ya pili, Hivyo wakati huo ndio waamini watafananishwa na Yesu kikamilifu. Kwa sasa waamini wanabadilishwa kila siku hatua kwa hatua (Utukufu hadi utukufu) lakini wakati utapotimia watafikia utukufu kamilifu. Paulo anaeleza kuhusu kuchukua picha hii katika muktadha wa ufufuo katika waraka wake kwa wakorintho.

1 WAKORINTHO 15

15.48  Kama alivyo yeye wa udongo, ndivyo walivyo walio wa udongo; na kama alivyo yeye wa mbinguni, ndivyo walivyo walio wa mbinguni.

15.49  Na kama tulivyoichukua sura yake yule wa udongo, kadhalika tutaichukua sura yake yeye aliye wa mbinguni.

WAEBRANIA 1:5-6

Waebrania inasema “Kwa maana alimwambia malaika yupi wakati wo wote, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa? Na tena, Mimi nitakuwa kwake baba, Na yeye atakuwa kwangu mwana? Hata tena, amletapo mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, asema, Na wamsujudu malaika wote wa Mungu.

Kwa waebrania uzaliwa wa kwanza wa Yesu NI CHEO AMBACHO MASIHI ALITABIRIWA ATAKUWA NACHO. CHEO HIKI NI CHA KIMAHUSIANO.

Kuelewa maana hii fuatilia kwa mtiririko jinsi mwandishi anavyotumia unabii wa kumhusu Masihi unaotoka katika kitabu cha Zaburi.

Muktadha. Yesu Kristo ni bora zaidi ya Malaika.

Anaanza kwa kuuliza swali  “Kwa maana alimwambia malaika yupi wakati wo wote, “Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa?” Na tena, “Mimi nitakuwa kwake baba, Na yeye atakuwa kwangu mwana?”

Jibu ni kwamba hakuna malaika yeyote Mungu alimwambia Maneno haya “Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa”  “Mimi nitakuwa kwake baba,Na yeye atakuwa kwangu mwana”.

Lakini haya  maneno Mungu aliyasema kumhusu Masihi miaka mingi kabla ya Yesu kuja.

Zaburi 2:2,7

2 Wafalme wa dunia wanajipanga, Na wakuu wanafanya shauri pamoja, Juu ya Bwana, Na juu ya masihi wake.

7 Nitaihubiri amri; Bwana aliniambia, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa.

Daudi anaandika kwamba MASIHI ameambiwa na Bwana kwamba “Wewe ndiwe Mwanangu, Mimi leo nimekuzaa”. Leo hii nimekuzaa inaonyesha ni cheo anachokipata masihi kisheria (kwa njia ya KUASILI au Kwa kiingereza inaitwa Adoption). Lugha hii KUASILI mtoto ni ngumu kidogo kwenye jamii yetu kwa kuwa jambo hili linafanyika kwa uchache. KUASILI ni kumchukua mtoto aliyezaliwa na mtu mwingine na kumfanya kuwa mwanao kwa njia ya kisheria. Mungu anamwambia Daudi, kwamba katika uzao wake kutatokea mashi ambaye Mungu atamfanya mwanae. Unabii ulianzia pale ambapo Daudi alitaka kumjengea Mungu hekalu, hivyo Mungu akamuahidi kumjengea yeye daudi nyumba ya kifalme milele/nasaba.

2 Samweli 7

14 Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; akitenda maovu nitamwadhibu kwa fimbo ya binadamu na kwa mapigo ya wanadamu;

15 lakini fadhili zangu hazitamwondoka, kama vile nilivyomwondolea Sauli, niliyemwondoa mbele yako.

16 Na nyumba yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele.

Daudi anaambiwa kwamba kupitia yeye atakuja MASIHI (Mwanae) ambaye Mungu atakuwa Baba yake naye atakuwa mwanae.

Hii ndio maana Yesu anaitwa Mwana wa Daudi ili kutimiza Unabii mwingi ambao Mungu aliusema kuhusu masihi ambaye ni YESU. Lakini pia ndio maana Mungu alifungua mbingu na kusema wazi kwamba “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye” (Mathayo 3:17, 17:5, Marko 9:7 na Luka 9:35). Baada ya maneno haya Wanafunzi wakapata uhakika kwamba Yesu ni MASIHI kwa kuwa walijua unabii. Hii ndio maana baada ya tukio hili wanaanza kumwambia lakini Ilitakiwa Eliya aje kwanza kabla ya wewe MASIHI kuja, Yesu anawajibu Eliya alishakuja (ambaye ni Yohana mbatizaji).

SASA TURUDI KATIKA MUKTADHA WA WAEBRANIA.

Baada ya kuonyesha kwamba MASIHI pekee ndiye Mungu alimpa cheo ambacho malaika hawakupewa kuitwa Mwanae. Sasa anaonyesha kwamba wakati Mungu anamleta MASIHI (Mzaliwa wa kwanza) ulimwenguni aliwaambia malaika wamsujudu.

Hata tena, amletapo mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, asema, Na wamsujudu malaika wote wa Mungu.”Hivyo Mwandishi wa waebrania ametumia cheo cha Uzaliwa wa kwanza Kikihusiana na UMASIHI wa Yesu. Kama ambavyo pia Mungu alitoa Unabii kwamba MASIHI atakuwa kwake mzaliwa wa kwanza katika zaburi nyingine ya 89.

Zaburi 89

26 Yeye ataniita, Wewe baba yangu, Mungu wangu na mwamba wa wokovu wangu.

27 Nami nitamjalia kuwa mzaliwa wangu wa kwanza, Kuwa juu sana kuliko wafalme wa dunia.

28 Hata milele nitamwekea fadhili zangu, Na agano langu litafanyika amini kwake.

29 Wazao wake nao nitawadumisha milele, Na kiti chake cha enzi kama siku za mbingu.

Hivyo Uzaliwa wa kwanza ni Cheo ambacho MASIHI aliahidiwa kupewa sio kwamba MASIHI atazaliwa wa kwanza katika familia yake bali cheo hiki kilikuwa kinaelezea mahusiano kati ya Mungu na MASIHI. Kwa wayahudi mtu kupewa hadhi ya uzaliwa wa kwanza (Mwanzo 25:29-34) ilikuwa ni kupewa mamlaka sawa na ile Baba aliyonayo nyumbani kwa kuwa mzaliwa wa kwanza alikuwa ndiye mrithi wa vitu vyote.

Ndio maana mwandishi wa waebrania anasema Yesu amechaguliwa kuwa mrithi wa vyote (1:2).

Hitimisho.

Biblia inapomtaja Yesu kuwa ndiye mzaliwa wa Kwanza haina maana moja kwenye kila mstari/aya. Kama tulivyoona kwamba katika Wakolosai 1:18, Ufunuo 1:5 na Warumi 8:29 Yesu ni mzaliwa wa kwanza kwa maana ya kwamba yeye ndiye mwanadamu wa kwanza kufufuka (baada ya kufa) na kuwa mtangulizi wa kuishi maisha mapya ya ulimwengu mpya ambayo waliokufa katika yesu watakapofufuliwa watayaishi/waamini wote watayaishi baada ya yesu kurudi tena.

Kwa wakolosai 1:15 ni mzaliwa wa kwanza kwa maana ya kwamba yeye ni mkuu (bora) juu ya viumbe vyote/uumbaji wote. Na kwa waebrania 1:5-6 yeye ni mzaliwa wa kwanza kwa maana ya kwamba yeye ndiye masihi aliyetabiriwa kuja kupitia ukoo wa Daudi na kuasiliwa na Mungu/kufanywa mwana na hivyo kuchaguliwa kuwa mrithi wa vitu vyote.

(Usichanganye uwana wa Yesu kwa sababu ya yeye kuwa ni masihi/kristo na uwana wa Yesu katika utatu mtakatifu wa Mungu, hivi ni vitu viwili tofauti).