Yuda – Mwongozo na Ufafanuzi

MWONGOZO WA KUSOMA WARAKA WA YUDA.

MAELEKEZO.

a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe mwamini mwenzangu unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako, usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.

b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa mstari kwa mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa kile tu kinachoweza kukuongoza wewe kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.

c. Pitia kila mistari inayowekwa katika mabano ili uelewe vizuri maandiko.

d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno basi tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo, utaona maelekezo ya ziada ya kukusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba husika.

e. Mpangilio wa kitabu wa mwongozo huu sio mpangilio wa mwandishi. Mpangilio katika mwongozo huu unakusaidia tu kuona kuhama kwa mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huo wala kwa mpangilio wa Sura na mistari.

UTANGULIZI.

Yuda aliandika waraka huu kwenda kwa waamini ambao hajataja waliishi maeneo gani ya kijiografia, Hii ndio maana waraka huu ni moja ya nyaraka zilizopewa kichwa cha “waraka wa….. kwa watu wote” katika tasfiri kadhaa za Biblia. Lakini ujumbe wa Yuda unaonyesha wazi ulikuwa kwa ajili ya waamini wa eneo/maeneo fulani waliokuwa na changamoto halisi ya kuwepo kwa waalimu wa uongo.

YUDA.

Yuda, mwandishi wa waraka huu alikuwa ni ndugu (kaka) wa Yakobo (1:1) na mmoja kati ya ndugu wanne wa Bwana wetu Yesu (Galatia 1:19, Marko 6:3 na Mathayo 13:55). Katika kuandika waraka huu hakuamua kutaja undugu wake na Bwana wake kama kaka yake Yakobo alivyofanya katika waraka wake (Yakobo 1:1). Yuda kama ndugu za Bwana Yesu wengine hakumuamini Yesu wakati wa huduma yake (Yohana 7:5) lakini alimuamini Yesu baada ya kufufuka kwake (Matendo 1:14). Yuda baada ya kuamini inaonekana alikuwa ni mmishenari/mwalimu wa kusafiri katika maeneo mbalimbali katika kuhubiri injili (1 Wakorintho 9:5).

KUSUDI LA WARAKA.

Yuda anasema wazi kwamba alikuwa anafanya bidii ya kuandika kuhusu Wokovu lakini akaghairi. Yuda anasema hakughairi kuandika kuhusu wokovu kwa kupenda, bali alilazimishwa na hali. Hali iliyomlazimisha Yuda ni uwepo kwa watu makafiri (wasiomcha Mungu) waliojiingiza kwa siri katika kanisa, ambao huibadili neema ya Mungu kuwa ufisadi (ruhusa ya kutenda maovu) na pia humkana yeye aliye peke yake Mola (Mkuu), na Bwana wetu Yesu Kristo[1]. Hivyo aliandika waraka huu kuwataka waamini kuishindania Imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu (3-4). Hivyo katika waraka huu Yuda anaeleza sifa, tabia, mwenendo na uhakika wa Hukumu ya watu hawa (waalimu wa uongo) kama ilivyotabiriwa wa manabii wa zamani kama vile Henoko na kama ilivyotabiriwa na mitume wa Bwana Yesu (5-19). Mbali na hayo Yuda anawaonyesha waamini namna ya kuishindania Imani waliokabidhiwa watakatifu mara moja tu (20-21).

MPANGILIO.

NambaMaandikoMaelezo
11-2Utangulizi wa waraka
23-4Sababu iliyopekea kuandikwa waraka na kusudi la waraka.
35-19Waalimu wa Uongo
 A5-10Uhakika wa Hukumu yao
B11-13Sifa zao
C14-16Utabiri wa Henoko kuhusu hukumu yao
D15-19Utabiri wa mitume wa Bwana Yesu
420-23Namna ya kuishindania Imani
524-25Maombi ya mwisho

MFULULIZO WA MAWAZO YA MWANDISHI.

Waraka huu una utangulizi wa waraka (1-2), ujumbe mkuu (3-23) na Mwisho wa waraka ambao ni maombi kwa Mungu (24-25). Utangulizi una utambulisho/anuani ya mwandishi (1a), utambulisho wa mwandikiwa (1b) na Salamu (2). Baada ya utangulizi huo wa warakaYuda anaanza ujumbe wake mkuu kwa utangulizi. Utangulizi wake wa ujumbe mkuu unaeleza hali iliyompelekea kuandika waraka huu na kusudi la waraka huu (3-4). Hali iliyompelekea Yuda kuandika waraka huu ni uwepo wa watu waliojingiza kwa siri ambao waligeuza neema ya Mungu kujihalalishia kutenda maovu (Ufisadi), na jambo hili atalieleza kwa urefu katika ujumbe mkuu (5-19). Kwa sababu ya hali hiyo Yuda aliandika waraka huu kuwataka waamini kuishindania Imani (kweli ya Mungu waliyoipokea kutoka kwa mitume) kwa nguvu, na jambo hili atalieleza tena kwenye kilele cha waraka huu (24-25).

Sehemu ya kwanza ya ujumbe mkuu (5-19) Yuda anaelezea kwanza uhakika wa hukumu kwa watu hawa (waalimu wa uongo). Uhakika huu anauelezea kwa kutumia mifano mitatu ya watu waliohukumiwa na Mungu katika historia kama ilivyoandikwa katika maandiko. Makundi haya ni kizazi cha wana wa Israeli kilichokombolewa kutoka misri (Hesabu 14), malaika walioacha enzi yao[2] na Sodoma, Gomora na miji iliyokuwa kando kando (Mwanzo 19). Na kila kundi Yuda ametaja sababu za kuhukumiwa kwao (5-7). Baada ya mifano hiyo kutoka kwenye maandiko Yuda anawataja watu hawa kwamba watapata Hukumu kama watu wa kwenye mifano aliyoitaja kwa kuwa nao(waalimu wa uongo)  wana maisha yafananayo na maisha ya watu wa kwenye mifano yake (8-10).[3] Baada ya kuelezea kuhusu uhakika wa hukumu wa watu hawa Yuda anataja sifa zao. Sifa yao ya kwanza yenye ole ndani yake ni kwamba wamechukua njia ya mifano mibaya ya watu watatu kutoka kwenye historia iliyopo kwenye maandiko. Watu hawa ni Kaini (Mwanzo 4:1-16, 1 Yohana 3:11), Baalamu (Hesabu 22-24) na Kora (Hesabu 16:1-35) (11)[4]. Baada ya mifano hiyo kutoka kwenye maandiko Yuda anataja sifa zao kwa kutumia lugha Mchanganyiko yaani anataja sifa zao kwa kutumia lugha ya picha na sifa halisi za namna wanavyoishi (12-13). Baada ya kutaja sifa za watu hawa, Yuda anawajulisha wasomaji wake kwamba, hukumu ya watu hawa ilishatabiriwa na Henoko. Henoko alitabiri hukumu ya Mungu kwa wasiomcha Mungu (Neno hili wasiomcha Mungu limetajwa mara tatu katika mstari wa 15) na hivyo watu hawa walitabiriwa kuhukumiwa kwa kuwa wao pia wana sifa hiyo hiyo ya kuto kumcha Mungu (14-16)[5]. Mwisho wa sehemu hii, Yuda anawakumbusha wapokeaji wa ujumbe wake kwamba mitume walishatabiri ujio wa watu hawa wenye kudhihaki na kufuata tamaa zao wenyewe za upotevu (17-19)[6].

Sehemu ya pili ya mjumbe mkuu (20-23) Yuda anasisitiza na kuelezea kusudi lake la kuandika waraka huu, yaani anasisitiza na kuelezea kuhusu kuishindania Imani. Yuda anawataka waamini waishindanie Imani kwanza kwa wao walioimara kujilinda na kujijenga zaidi (20-21) na pia kuwasaidia na kuwaokoa ambao tayari wameathiriwa na watu hawa waovu waliojiingiza kwa siri (22-23). Mwisho wa waraka huu Yuda anamaliza kwa Maombi kwa Mungu (24-25).

MFANANO WA WARAKA WA YUDA NA WARAKA WA PILI WA MTUME PETRO.

Ukisoma waraka wa Yuda na waraka wa pili wa Petro si vigumu kugundua kwamba kuna mfanano wa matumizi ya Lugha. Jedwali hapo chini litakusaidia kuona mfanano wa Yuda na Petro katika matumizi ya Lugha.

YUDAMANENO2 PETRO
4hukumu yao tangu zamani2:3
4wakimkana hata Bwana2:1
6Malaika katika vifungo vya giza2:4
7Mfano wa Hukumu ya Sodoma na Gomora2:6
8kuyatukana matukufu2:11
9Kuleta mashitaka2:11
10Wakikufuru/tukana katika mambo wasiyoyajua2:12
11Mfano wa Baalamu2:15
12karamu zenu za upendo2:13
12ni mawingu yasiyo na maji, yachukuliwayo na upepo2:17
18siku za mwisho watakuja na dhihaka zao watu wenye kudhihaki, wafuatao tamaa zao wenyewe3:3



FOOTNOTES

[1] Namna watu hawa wanamkana yeye aliye peke yake mkuu na Bwana wetu Yesu Kristo sio kwa mafundisho au ukiri wao, bali kwa namna wanavyoishi, Hii ndio maana Yuda anasema wako kwa siri. Lakini pia ndio maana Yuda anaeleza zaidi namna wanavyoishi kuliko wanavyosema au kufundisha.

[2] Hawa malaika walioacha enzi yao wenyewe Yuda hajataja kwa wazi ni tukio gani hasa analolizungumzia, tukio hili linaweza kuwa la kuasi kwa shetani na malaika zake au tukio la wana wa Mungu kuja kuzaa na wana wa wanadamu (Mwanzo 6:1-6). Kwa kuwa Yuda ananukuu kitabu cha 1 Henoko katika mistari ya 14-15 na katika kitabu hicho hicho wana wa Mungu wa Mwanzo 6:1-6 wanaelezwa kuwa ni malaika hivyo itakuwa sahihi kusema Malaika Yuda anaowazungumzia ni wana wa Mungu wa Mwanzo 6:1-6.

[3] Zingatia maelezo Yuda anayoyasema kuhusu maisha/tabia za watu hawa. Anasema 1. huutia mwili uchafu 2. hukataa kutawaliwa 3. kuyatukana matukufu.

[4] Sifa ya kaini ni uuaji, sifa ya Baalamu ni kupenda kipato cha aibu/udhalimu na sifa za kora ni uasi hivyo hizo ni sifa za watu hawa Yuda anaowaelezea

[5] Unabii huu wa Henoko unapatikana katika kitabu cha 1 Henoko kitabu ambacho hakipo katika Biblia zetu (1 Henoko 1:9)

[6] Ilikuwa ni kawaida mitume kuwaonya waamini kuhusu ujio wa watu kama hawa (Matendo 20:17-38, 1 Timotheo 4:1-20) lakini maneno haya Yuda aliyoyasema yanafanana kabisa na maneno aliyoyasema Mtume Petro katika waraka wake wa pili (2 Petro 3:3) ambao unafanana sana na waraka huu. Hivyo inawezekana Yuda alinukuu maneno haya ya Petro japo hakuna uhakika kwamba waraka wa Yuda uliutangulia waraka wa pili wa mtume Petro.

UFAFANUZI WA WARAKA WA YUDA.

Unakuja hivi karibuni…….