MWONGOZO WA KUSOMA UJUMBE WA NABII ZEKARIA.
MAELEKEZO.
a. Huu ni mwongozo wa kukusaidia wewe mwamini mwenzangu unapoamua kusoma kitabu hiki. Soma mwongozo huu ukiwa unasoma Biblia yako, usifanye mwongozo huu kuwa mbadala wa kusoma Biblia.
b. Mwongozo huu hautoi ufafanuzi wa mstari kwa mstari wa kile mwandishi anachosema bali unatoa ufafanuzi wa kile tu kinachoweza kukuongoza wewe kusoma mwenyewe ili upate kuelewa.
c. Pitia kila mistari inayowekwa katika mabano ili uelewe vizuri maandiko.
d. Kila utakapoona namba juu/mbele ya neno basi tafuta namba hiyo husika chini ya ukurasa huo, utaona maelekezo ya ziada ya kukusaidia kuelewa sehemu husika iliyobeba namba husika.
e. Mpangilio wa kitabu wa mwongozo huu sio mpangilio wa mwandishi. Mpangilio katika mwongozo huu unakusaidia tu kuona kuhama kwa mawazo ya mwandishi kutoka hoja moja kwenda nyingine. Waandishi wa Biblia hawakuandika kwa mpangilio huo wala kwa mpangilio wa sura na mistari.
UTANGULIZI.
Nabii Zekaria ni nabii aliyeleta ujumbe wake wakati wa utumishi wa Nabii Hagai. Nabii Hagai alitoa unabii kwa muda mfupi, na hivyo kumuachia Nabii Zekaria jukumu la kuendelea na kazi hii ya kinabii kwa taifa la Mungu. Hii ndio sababu kitabu cha Nabii Zekaria kimefuata kitabu cha Nabii Hagai katika Biblia zetu. Nabii Zekaria pia alikuwa mmoja wa manabii wa Israeli waliotoka katika ukoo wa kikuhani. Ukoo wake (Zekaria 1:1, 7; Ezra 5:1, 6:14) unatambulishwa na Nehemia kama ukoo wa kikuhani (Nehemia 12:1-4). Asili yake ya kikuhani inaweza kuwa sababu ya mkazo wake juu ya mambo ya hekalu na ukuhani katika kitabu hiki.
MUKTADHA WA KIHISTORIA WA UJUMBE WA NABII ZEKARIA.
Baada ya utawala wa Suleimani kuisha, taifa la Israeli liligawanyika na kuwa mataifa mawili; Israeli na Yuda (1 wafalme 12:1-22). Israeli walianza kuabudu sanamu mara tu baada ya kutengena na hekalu la Jerusalem (1 wafalme 12:23-33). Hivyo, Mungu akawatuma manabii kuwaonya Israeli kwa mabaya walioamua kuyafanya. Kati ya manabii wengi Mungu aliowatuma walikuwepo manabii Hosea na Amosi. Kwa kuwa Israeli haikusikia sauti ya Bwana kupitia manabii, Mungu akaruhusu Israeli kupigwa na kuchukuliwa mateka na dola ya Ashuru. Dola ya Ashuru iliwatawanya Waisraeli kwenye maeneo mbalimbali na kuwachukua watu wengine kutoka kwenye maeneo mbalimbali na kuwaleta kwenye ardhi ya Israeli, na hivyo Israeli ikapoteza utaifa wake hapo (1 Wafalme 17).
Pamoja na hilo, taifa la Yuda halikujifunza kutoka kwa ndugu zao, nao walifanya mabaya mbele za Mungu (1 Wafalme 17:19). Mungu pia aliwatuma manabii kwa taifa la Yuda kuwaonya kutokana na dhambi zao hasa ibada ya sanamu na udhalimu wa kijamii/ukiukaji wa haki katika jamii (1 wafalme 17:13). Kati ya manabii wengi ambao Mungu aliwatuma wapo Mika, Isaya na Yeremia. Kwa kushindwa kutubu Mungu aliruhusu taifa la Yuda kupigwa na watu wake kupeleka utumwani Babeli kwa awamu mbili; awamu ya kwanza chini ya ufalme wa Yehoyakimu (2 Wafalme 23:34-24:1-7), na awamu ya pili wakati wa ufalme wa Yehoyakini (2 Wafalme 24:8-20). Pamoja na watu wengine kubaki katika Yuda na mfalme Nebukadreza kuweka mfalme mwingine juu ya Yuda, Israeli waliobaki hawakumrudia Mungu na hivyo Nebukadreza akarudi tena kuupiga mji wa Jerusalemu na kuuchoma kwa moto (2 Wafalme 25). Jambo hili lilitokea baada ya nabii Ezekiel kutabiri hivyo kwa wale waliokuwa utumwani tayari. Yeye mwenyewe alitabiri akiwa utumwani. Mpaka wakati huu Israeli na mataifa mengine mengi yalikuwa yanatawaliwa na dola ya Babeli.
Kama Mungu alivyotabiri kupitia kinywa cha Nabii Danieli (na Isaya pia) kwamba atainua ufalme mwingine baada ya Babeli, basi Mungu akainua dola ya Umedi na Uajemi (Danieli 2,7 na 8). Umedi na Uajemi ukaipiga dola ya Babeli, na hivyo mateka wote na makoloni yote ya Babeli yakawa chini ya utawala wa Umedi na Uajemi. Mungu akatumia utawala huu kuwaruhusu taifa la Yuda kurudi nyumbani kwao na kuwa na shughuri zao za ibada kama ilivyokuwa mwanzo (2 Nyakati 36, Ezra 1:1-4). Hii ni baada ya taifa la Yuda kuwa utumwani Babeli kwa muda wa miaka sabini kama ilivyotabiriwa na nabii Yeremia (Yeremia 25:1). Sera ya utawala wa Umedi na Uajemi uliwaruhusu mateka kurudi kwenye mataifa yao na kuendelea na shuguri zao za kuabudu pamoja na kwamba waliendelea bado kuwa chini ya utawala wao.
Waliporuhusiwa kurudi nyumbani, watu wa Yuda hawakurudi wote kwa wakati mmoja; walirudi kwa makundi matatu tofauti. Kundi la kwanza lilirudi chini ya uongozi wa Sheshbaza na Zerubabeli. Kusudi la kundi hili lilikuwa ni kujenga Hekalu kwanza (Ezra 1-6). Baada ya hatua za kwanza za ujenzi, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa msingi (Ezra 3:8-13), upinzani kutoka nje na ndani ulisimamisha kazi kwa muda wa miaka kumi na minne (14). Kwa kusimamishwa kwa kazi ya Hekalu, watu walianza kufuata masilahi yao binafsi na kujijengea majumba mazuri ya kuishi huku wakisahau kabisa ujenzi wa Hekalu waliouacha njiani. Hapo ndipo Mungu alipomtuma nabii Hagai kuwarudisha Yuda kwenye ujenzi wa Hekalu. Baada ya nabii Hagai, nabii Zekaria akaendelea na kazi hiyo hiyo, na hatimaye Hekalu likajengwa na kukamilika miaka minne baadaye (Ezra 6:14-15). Kundi la pili la Waisraeli walirudi wakiwa katika uongozi wa Ezra, ambaye alirudisha usomaji na ufuataji torati ya Musa (Ezra 7-10). Kundi la tatu, walirudi wakiwa na uogozi wa Nehemia, ambaye alirudi kwa lengo la kujenga tena ukuta wa Yerusalemu uliobolewa (Nehemia 1-13).
Hivyo, Nabii Zekaria alitoa ujumbe wake wakati ambapo watu wa Yuda walikuwa wametelekeza ujenzi wa hekalu. Hii ilikuwa katika kipindi ambacho kundi la pili na la tatu la watu wa Yuda bado hawajarudi katika taifa lao, na hivyo Ezra na Nehemia walikuwa hawajarejea. Katika wakati huu, nabii Zekaria aliendeleza kazi iliyoanzishwa na nabii Hagai.
UJUMBE MKUU WA NABII ZEKARIA.
Ujumbe wa Zekaria ni ujumbe wenye lengo kuu la kuwatia moyo watu wa Yuda waliorudi kutoka utumwani katika kazi yao ya ujenzi wa hekalu. Kupitia maono mbalimbali, Mungu anatoa matumaini ya urejesho kwa watu wake, na kupitia hotuba na mashairi mbalimbali, Mungu anatangaza kuwarudia na kuwalinda watu wake. Ujumbe wake unaanza na wito wa toba; Mungu anaahidi kuwarudia watu wake ikiwa watamrudia Yeye (Zekaria 1:2-6). Maono ya Zekaria yanasisitiza ulinzi wa Mungu juu ya Yerusalemu na mpango wake wa kukaa kati ya watu wake (Zekaria 2-6). Kwa sababu ya ahadi hizo za Mungu, maombolezo ndani ya taifa la Mungu yatageuzwa kuwa sherehe zitakazoungwa mkono na mataifa mengine (Zekaria 7-8). Mungu pia atawapiga maadui wote wa Israeli, atawarudisha watu wake wote waliosalia uhamishoni, na hatimaye atamleta Masihi wake, Mfalme wa amani au Mchungaji mwema (Zekaria 9-11). Mwisho, ujumbe wa Zekaria unatangaza ujio wa siku njema za baadaye katika taifa la Mungu na ushindi wa Mungu juu ya ulimwengu wote (Zekaria 12-14).
MPANGILIO WA KITABU.
Namba | Maandiko | Maelezo |
1 | 1:1-6 | Utangulizi: Nirudieni mimi |
2 | 1:7-17 | Maono ya kwanza: Bwana anawarudia watu wake |
1:18-21 | Maono ya pili: Maadui wa Yuda wataangushwa | |
2:1-13 | Maono ya tatu: Jerusalem italindwa na Bwana | |
3:1-10 | Maono ya nne: Kuhani mkuu kushitakiwa | |
4:1-14 | Maono ya tano: Hekalu litajengwa kwa Roho wa Bwana | |
5:1-4 | Maono ya sita: Hukumu kwa mwivi na mwongo | |
5:5-11 | Maono ya saba: Uovu kuondolewa katika Israeli | |
6:1-8 | Maono ya nane: Nguvu za Bwana duniani kote | |
6:9-15 | Chipukizi atatawala | |
3 | 7-8 | Maombolezo kugeuzwa kuwa sherehe |
4 | 9-10 | Mashairi ya ahadi za urejesho |
5 | 11 | Mchungaji mwema na kondoo wake |
6 | 12-13 | Ushindi wa taifa la Mungu na utakaso wa watu wake |
7 | 14 | Ushindi wa Mungu juu ya mataifa |
MFULULIZO WA MAWAZO YA MWANDISHI.
Nabii Zekaria anaanza kutoa ujumbe wake mwezi wa nane, mwaka wa pili wa mfalme Dario. Ujumbe wake ni mwito wa Mungu kwa watu wa Yuda kumrudia na kuishi kulingana na agano. Mungu anawaita watu wa Yuda waliorejea kutoka uhamishoni kumrudia ili awarudie. Anawakumbusha kuhusu baba zao ambao walionywa na manabii lakini hawakusikiliza, hivyo wakaenda uhamishoni. Kupelekwa uhamishoni kulithibitisha kwamba neno la Mungu ni kweli. Mungu anawataka kizazi cha sasa kisiwe kikaidi kama kile cha awali. (1:1-6).
Baada ya utangulizi huo, ujumbe wa kitabu hiki unafuatiwa na maono ya aina nane aliyoyaona nabii Zekaria usiku mmoja. Maono haya aliyaona miezi mitatu baada ya ujumbe wake wa kwanza. Maono ya kwanza ni kwa ajili ya kuwafariji Yuda kwamba Bwana anawarudia; Bwana atawaangamiza mataifa ambao sasa wanakaa kwa amani na utaujenga mji wa Yerusalemu na hekalu ndani yake. Zaidi ya hayo, Bwana ataipa miji ya watu wa Yuda mafanikio ya mali na hivyo miji hiyo itatanuka (1:7-17). Maono ya pili ni maono ya faraja pia kwa watu wa Yuda. Katika maono haya, Mungu anamuonyesha nabii Zekaria kwamba dola zote nne zilizohusika kuwatawanya taifa la Israeli zitapigwa na kuangushwa, hivyo Yuda itakuwa huru kweli kweli (1:18-21). Katika maono ya tatu, nabii Hagai anaona malaika anaupima mji wa Jerusalem na anapata tangazo kutoka kwa Bwana kwamba, Jerusalem utakuwa na watu wengi, utajengwa na utalindwa na Mungu mwenyewe. Mungu atatimiza hili kwa kuwapiga maadui wa Yuda na mwishoe mataifa mengi yatajiunga kwa Bwana (2:1-13). Kumbuka maono haya yote yanakuja wakati mji wa Jerusalem haujajengwa upya, hekalu liko kwenye msingi na watu wametoka utumwani, hivyo hawana rasilimali za kutosha kutimiza kazi hizi.
Baada ya maono ya ahadi ya urejesho wa taifa, nabii Zekaria alimwona Kuhani Mkuu Joshua akiwa na mavazi machafu (yakiwakilisha uovu), mbele ya mshitaki Ibilisi. Pamoja na kushitakiwa, Bwana aliamua kuuondoa uovu huo na kumpa Joshua mavazi mazuri. Joshua alitakiwa sasa kuenenda kwa kufuata maagizo ya Bwana ili aendelee kumkaribia. Joshua pia alijulishwa kwamba yeye na makuhani wengine ni ishara ya Chipukizi ajaye, ambaye ni Masihi (3:1-10). Haya yalikuwa maono ya nne ya nabii Zekaria.
Baada ya maono hayo kumhusu Kuhani Mkuu Joshua, maono ya tano yanamhusu sana Liwali Zerubabeli. Nabii Zekaria anaona kinara cha taa cha dhahabu chenye taa saba juu yake na mirija saba iletayo mafuta. Kinara hiki cha taa kimezungukwa na mizeituni miwili; mmoja upande wa kushoto na mwingine upande wa kulia. Maono haya yalikuwa ni kumjulisha Liwali Zerubabeli kwamba kazi ya ujenzi wa hekalu haitafanikiwa kwa sababu ya nguvu za kisiasa wala uwezo wa kiuchumi, bali kwa sababu ya uwepo wa Roho wa Mungu. Kwa kuwa Zerubabeli ndiye aliyeweka msingi wa jengo la hekalu, Mungu anamjulisha nabii Zekaria kwamba Zerubabeli huyo huyo ndiye atakayekamilisha kazi hii kwa kuwa hakuna upinzani utakaomshinda. Katika kazi hii, Zerubabeli hatakuwa peke yake; atakuwa na Kuhani Mkuu Joshua. Kwa pamoja, wao ndio ile mizeituni miwili iliyoko kushoto na kulia kwa kinara cha taa (4:1-14).
Maono ya sita ya nabii Zekaria katika usiku ule yalikuwa kuhusu kitabu kilichopaa (Gombo). Kitabu hiki kilikuwa kimeandikwa pande zote mbili. Mungu anampa maono haya Zekaria kumjulisha kwamba waongo na wezi watahukumiwa na sheria yake ambayo iko katika nchi yote (5:1-4). Baada ya maono hayo, nabii Zekaria akaona kikapu cha kupimia (Efa) ambacho kilikuwa kimefunikwa na mfuniko wa madini ya risasi wenye uzito wa talanta moja (kama kilo 30). Baada ya kufunuliwa mfuniko huo, nabii akamuona mwanamke ndani yake. Mwanamke huyu aliwakilisha uovu. Baada ya kufunikwa tena, mwanamke huyu alibebwa na wanawake wawili mpaka Babeli (Shinari). Maono haya yalionyesha kuondolewa kwa uovu kutoka katika nchi ya Yuda (5:5-11).
Katika maono ya mwisho, Zekaria anaona magari manne yanayovutwa na farasi wa rangi nne tofauti. Magari haya yanatoka kwenye milima miwili ya shaba. Magari haya yanawakilisha roho nne za mbinguni zinazosimama mbele ya Mungu na sasa ziko tayari kwenda duniani kote. Maono haya yanawakilisha kuenea kwa nguvu za Bwana duniani kote (6:1-8). Maono ya nabii Zekaria yanafikia mwisho kwa Mungu kumtuma kutoa unabii kwa watu wa Yuda; unabii unaambatana na tendo la ishara. Unabii huu ulikuwa ni kutangaza kwa Joshua na watu wanne waliotoka utumwani (Heldai, na Tobia, na Yedayana Sefania), kwamba Bwana atamuinua chipukizi ambaye atajenga hekalu lake na atakuwa mtawala wa watu wa Mungu. Chipukizi atakuwa pamoja na kuhani katika kazi yake; kati yao kutakuwa na amani. Unabii huu ulitolewa baada ya ishara ya kumvalisha taji kuhani mkuu Joshua kufanywa na nabii Zekaria (6:9-15).
Baada ya miaka miwili tangu siku nabii Zekaria alipoona maono nane ndani ya usiku mmoja, alipokea ujumbe kutoka kwa Bwana. Neno la Bwana lilimjia nabii Zekaria baada ya watu kutoka Betheli kwenda kuwauliza makuhani na manabii kama waendelee kufunga kwa ajili ya kuuombolezea mji wa Jerusalemu (na hekalu) uliobomolewa, kama walivyokuwa wakifanya walipokuwa Babeli kwa miaka yote sabini (7:1-3). Kabla ya kutoa jibu la moja kwa moja, Mungu anawahoji taifa zima: Je, walipofanya ibada zao za kufunga au walipokula, walifanya kwa ajili yake, au walifanya kwa ubinafsi wao wenyewe? (7:4-6). Swali hili lina jibu; jibu ni kwamba walifanya kwa ubinafsi na wala haikuwa ibada njema kwa Bwana. Baada ya kuwaonyesha jinsi mioyo yao ilivyo, Mungu anawakumbusha kwamba kilichowafanya waende utumwani Babeli ilikuwa ni kutokusikia sauti yake iliyosema na taifa kupitia manabii wake wa kwanza (7:7-14). Pamoja na historia hiyo mbaya, Mungu ameamua kuurudia Jerusalemu, na hivyo utakaliwa na watu wake wote wakiwa na afya njema; watu ambao atawarejesha na ambao tayari ameshawarejesha (8:1-8). Mungu pia anasema ataubariki mji wa Jerusalemu kwa amani, mazao bora, na hali ya hewa njema kama kizazi cha sasa kitasikiliza sauti yake (8:9-15), kwa kutenda mema tofauti na mabaya ya wazazi wao (8:16-17). Baada ya maelezo hayo mazuri, Mungu anajibu swali lililoulizwa; Mungu anasema miezi yao ya kufunga itageuzwa na kuwa sikukuu zenye furaha na shangwe. Kwa sababu ya urejesho huo ndani ya Jerusalemu, mataifa wataalikana na kuja Jerusalemu kumuabudu Mungu wa kweli (8:18-23).
Baada ya hotuba hiyo ndefu ya Mungu, kitabu cha nabii Zekaria kinaingia kwenye sehemu yenye uwingi wa mashairi[1] na matendo ya ishara[2]. Sehemu hii inaanza na shairi linaloelezea hukumu ya Mungu juu ya majirani wa Yuda. Mungu ataihukumu miji ya Hadraki, Dameski, Hamathi, Tiro, pamoja na Sidoni. Kwa sababu ya hukumu hiyo, miji mingine itaogopa, lakini Mungu atailinda mipaka ya nyumba yake, Israeli/Yuda (9:1-8). Shairi la pili ni mwito kwa watu wa Yuda kufurahi kwa kuwa mfalme anakuja ambaye atatawala kwa amani katika Yerusalemu (9:9-10). Katika shairi la tatu, Mungu anatangaza kuwarudisha nyumbani watu wa Yuda ambao hawajarudi, na anawahimiza walioko Babeli kurudi nyumbani kwa sababu atawapa baraka maradufu na hatimaye atawatumia kuwapiga Wagiriki. Mungu atafanya hivi kwa sababu ya agano lake la damu alilofanya na taifa lake (9:11-17).
Shairi la nne ni shairi la makalipio kwa viongozi (wachungaji/mbuzi dume) na ahadi ya urejesho kwa watu wa Yuda. Mungu anawaita watu kumuomba yeye huku akiwakataza kufuata sanamu (vinyago na waaguzi) ambazo zinawafanya kupotea. Ufuataji wa sanamu ni matokeo ya viongozi waovu, na hivyo Mungu anasema atawahukumu viongozi hao (10:1-3). Tofauti na viongozi hao, ndani ya Yuda Mungu atamwinua kiongozi mwenye sifa kama jiwe la pembeni, kama msumari unaoshikilia hema, kama upinde wa vita, ambaye kutoka kwenye ukoo wake watatoka watawala wengi. Kupitia kiongozi huyo, watu wa Yuda na Israeli watakuwa mashujaa, na hivyo watashinda vita dhidi ya maadui zao (10:4-7). Mwisho, Mungu anatangaza kuwarudisha watu wake wote kutoka mataifa yote aliyowafukuzia (10:8-12). Mataifa haya ni kama vile Misri, Ashuru, Gileadi na Lebanoni. Kwa kutumia lugha ya picha ya miti (kama vile Mierezi, misunobari na mialoni), Mungu anatangaza hukumu yake juu ya viongozi wa taifa la Lebanoni. Kwa kuwa Lebanoni itahukumiwa na Mungu pamoja na uimara wake, hivyo mataifa mengine yanatakiwa kuomboleza. Kama mwenye nguvu atapigwa kiasi hicho, basi wasio na nguvu wanatakiwa kuomboleza (11:1-3).
Kabla ya kuendelea na mashairi, Mungu anamtuma nabii Zekaria kufanya tendo la ishara. Tendo hili liko katika pande mbili. Katika upande wa kwanza, Mungu anamwambia Zekaria akachunge kondoo walio tayari kuchinjwa. Kondoo hao walikuwa wanachungwa na wachungaji waovu. Zekaria akawachunga kwa fimbo mbili; moja ni Fadhili (Neema) na ya pili ni Umoja (Vifungo). Kwa kuchoshwa na kondoo hao, Zekaria akaamua kuwaacha wajichunge wenyewe na hatimaye akavunja fimbo zake mbili. Tendo hili linaonyesha uhusiano wa Mungu na watu wake ulivyokuwa na jinsi ulivyovunjika (11:4-14). Katika upande wa pili, Mungu anamwambia Zekaria awe mchungaji mwovu, mchungaji alaye kondoo badala ya kuwatunza (11:15-16). Baada ya Zekaria kufanya tendo hili, Mungu anatoa ole kwa wachungaji waovu (11:17).
Baada ya matendo hayo ya ishara, Mungu anatangaza kwamba ipo siku ambayo maadui wote wa Yerusalemu wataangamizwa, lakini mji wa Yerusalemu utahifadhiwa. Wakati huo, Mungu pia ataimarisha ukoo wa Daudi ili uwaongoze watu wa Yuda (12:1-9). Katika kipindi hicho taifa lake Mungu litaingia kwenye maombi na maombolezo. Watu wote, katika rika, hadhi, na jinsia zao, watamwombolezea yeye waliyemchoma, ambaye ni Mungu mwenyewe. Maombolezo haya yatasababishwa na Mungu, kwa kuwapa roho ya neema na maombi watu wa Yuda (12:10-14). Katika kipindi hicho hicho, Bwana anaahidi kutakasa watu wa Yuda. Utakaso huu unahusisha kuondoa sanamu na manabii wa uongo kutoka katika taifa. Watu watajitoa kwa Mungu kwa moyo wote kiasi kwamba hata wazazi wa nabii wa uongo watakuwa tayari kumuua mwana wao. Manabii wa uongo watajaribu kuficha ujanja wao, wakidai kwamba wao si manabii kabisa (13:1-6). Katika kipindi kingine, Zekaria anatabiri kwamba mchungaji wa Mungu juu ya watu wake atapigwa. Kupigwa kwake kutasababisha theluthi mbili ya watu kuangamizwa, na theluthi moja itakayosalia itatakaswa na kuimarishwa na Bwana (13:7-9).
Ujumbe wa Zekaria unafikia mwisho kwa utabiri kuhusu ujio wa siku ya hasira ya Bwana. Siku hii itaanza na Yerusalemu kutekwa na watu wake kupigwa, kutendewa jeuri na nusu yao kupelekwa utumwani (14:1-2). Baada ya kipigo hicho, Bwana ataingilia kwa kuyapiga mataifa yaliyoipiga Israeli. Bwana atatengeneza njia kwa kupasua mlima ili nusu ya watu wake waweze kukimbia kujinusuru (14:3-6). Siku hii itaishia kwa Bwana kushuka na jeshi la malaika wake kwa ajili ya kubadilisha kipigo cha Yerusalemu kuwa ushindi wake. Bwana atautawala Yerusalemu na ataufanya kuwa na amani huku akiwapiga mataifa yote yaliyouvamia (14:7-15). Hatimaye, Yerusalemu utakuwa mji mtakatifu kweli kweli, na watu watakaosalia katika mataifa (baada ya kipigo) watakuwa wakienda Yerusalemu kila mwaka kusherehekea Sikukuu ya Vibanda pamoja na Wayahudi (14:16-21).
FOOTNOTES
[1] Zingatia kwamba sifa ya ushairi ni matumizi makubwa ya lugha ya picha, Hivyo sio kila neno lina maana ya kawaida katika ushairi.
[2] Matendo ya ishara ni matukio manabii walikuwa wanafanya au wanaambiwa kufanya huku yakiwa yanatabiri nini kitatokea au yanaelezea uhalisia wa hali inayoendelea. Hivyo, matendo haya yalikuwa ni unabii kwa njia ya matendo.
Unakuja hivi karibuni…